Kesi ya mauji dhidi ya mwanafunzi wa chuo kikuu cha Rongo Sharon Otieno itaendelea juma lijalo licha ya washukiwa wakuu kwenye kesi hiyo gavana wa Migori Okoth Obado na Michael Oyamo kutaka ihairishwe kwa kuhofia corona.
Jaji Cecilia Githua ameagiza kesi hiyo kuendelea kuanzia Jumatatu ijayo Julai 12 hadi Julai 15 katika mahakama ya Milimani.
Kupitia kwa mawakili wao Kioko Kilukumi na Profesa Tom Ojienda, wawili hao walitaka kesi hiyo kuhairishwa kwa mwezi mmoja kwa sababu kaunti ya Migori ni miongoni wa kaunti zilizoathirika zaidi na corona.
Obado na Oyamo walikuwa wanahoji kwamba hatua hiyo itawalinda dhidi ya kupatwa na ugonjwa huo.
Ombi hilo lilipingwa na wakili wa familia ya marehemu Daniel Njoroge kwa misingi kwamba kesi hiyo imekuwa ikijikokotas kwa miaka mitatu tangu Sharon aliyekuwa mja mzito kuuawa.
Upande wa mashtaka vile vile umepinga ombi hilo kuhairisha kesi hiyo.