Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga anasisitiza kwamba shida kubwa inayokumba taifa hili ni wizi wa pesa za umma.

Odinga akihutubu kwenye mazishi ya mama Esther Githaiga huko Nyeri amesema kinachostahili kufanywa ni kuziba mianya inayotumiwa na baadhi ya viongozi kuendeleza ufisadi.

Waziri huyo mkuu wa zamani ameshikilia kwamba mchakato wa kubadilisha katiba kupitia BBI utaendelea baada ya kutiwa breki na mahakama.

Mbunge wa Kieni Kanini Kega ametumia fursa hiyo kuashiria kwamba watamuunga mkono Odinga iwapo wataelekezwa na rais Uhuru Kenyatta.

Marehemu alikuwa mamake Agnes Mumbi ambaye ni mwanachama wa kamati ya nidhamu katika chama cha ODM.