Hatimaye Kenya na Marekani wameafikia makubaliano ya kutanzua mgogoro ambao umesababisha kukwama kwa dawa za kuzuia makali ya virusi vya HIV katika bandari ya Mombasa tangu mwezi Januari mwaka huu.

Afisa mkuu mtendaji wa baraza la kitaifa la kupambana na ugonjwa huo (NACC) Ruth Masha katika taarifa amesema mzozo huo umetatuliwa kufuatia kuundwa kwa kamati ya pamoja kuangazia maswala ibuka.

Amesema mzigo wenye dawa hizo sasa utaruhusiwa kuondoka bandarini na hivyo kutoa fursa ya kuanza kusambazwa kote nchini.

Mgogoro huo umehatarisha maisha ya wagonjwa wengi wanaoishi na virusi vya HIV ambao walikosa kupata dawa walipotembelea vituo mbalimbali vya afya.