Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC imeshikilia kuwa ilikuwa na makamishna wa kutosha kisheria wakati ilikagua na kuidhinisha saini za kuunga mkono mswada wa kufanyia katiba marekebisho wa BBI.
Kupitia kwa wakili wake Githu Muigai, tume hiyo chini ya uenyekiti wa Wafula Chebukati imeliambia jopo la majaji saba wanaosikiliza rufaa ya BBI kuwa sheria ambayo majaji wa mahakama kuu walitumia kuafikia uamuzi wao haijakuwa ikitumika.
Badala yake, Muigai ameliambia jopo hilo ambalo linaongozwa na Rais wa mahakama ya rufaa Daniel Musinga kuwa kipengee cha 250 cha katiba kinaruhusu tume huru kikatiba kuendesha shughuli zake na makamishna watatu au zaidi.
Kuhusiana na zoezi la kuidhinisha saini zilizowasilishwa kwao iwapo ni ghushi au la, wakili Gumbo Eric anayewakilisha IEBC amesema wakenya walipewa fursa ya kudhibitisha taarifa zao kwa mujibu wa sheria.