Rais Uhuru Kenyatta amewaongoza viongozi mbalimbali kumuomboleza mfanyibiashara tajika Chris Kirubi aliyefariki baada ya kuugua ugonjwa wa saratani.
Uhuru kwenye ujumbe wake amemtaja kama mfanyibiashara aliyefaulu kwenye biashara nyingi aliyoanzisha na kwamba mchango wake katika uchumi wa Kenya utakumbukwa.
Naibu rais William Ruto amesema Kirubi alitambulika pakubwa na maono yake katika maswala ya biashara ambaye ubunifu wake utabakia kuigwa na wengi.
Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga amemtaja marehemu kama rafiki wa karibu na aliyejitolea kuwasaidia waliohitaji msaada wake.
Wengine waliotuma risala zao za rambi rambi ni Musalia Mudavadi kiongozi wa chama cha ANC, mwenzake wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, spika wa bunge wa la kitaifa Justine Muturi, maseneta Moses Wetangula (Bungoma) na Gavana wa Mombasa Hassan Joho.