Maafisa wa polisi katika kaunti ya Kakamega wanachunguza mauaji ya walinzi watatu wa Shule ya Upili ya Wavulana ya Kivaywa usiku wa kuamkia Alhamisi.

OCPD wa eneo hilo Thomas Ototo anasema watatu hao waliuawa na wezi ambao waliiba mali ya thamani isiyojulikana ikiwemo tarakilishi na runinga.

Miili ya watatu hao Edward Malala 40, Henry Khaoya 55 na Evans Wanyonyi 56, ilipatikana imetapakaa katika ua wa shule hiyo ikiwa na majeraha ya panga na visu.

Miili yao inahifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Lugari huku maafisa wa usalama wakiahidi kuwakamata wahusika.