Kwa mara nyingine tena, maafisa wa usalama wametibua mkutano wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachohusishwa na naibu rais William Ruto mjini Mombasa.

Inaarifiwa kwamba Polisi wakiongozwa na kamanda wa Polisi Nyali Daniel Masaba walifika kulikokuwa na mkutano huo na kumuagiza kila mtu kuondoka.

Iliwalazimu wagombea mbalimbali waliokuwa wanakutana kupanga mikakati ya kuboresha chama hicho mashinani kuondoka Polisi wakisema kwamba hawakujulishwa mapema.

Itakumbukwa kwamba Polisi Jumatatu iliyopita walitibua mkutano sawa na huo huko Meru kwa madai kuwa waandalizi wake hawakuwa na kibali.

Katibu wa UDA Veronica Maina alikashifu hatua hiyo akisema hawakuhitaji kibali kuandaa mkutano huo.

Kupitia taarifa, chama hicho kimewalaumu Polisi kutokana na kile kimetaja kama kutumiwa kuwanyanyasa bure.