Jopo la majaji saba litasikiliza na kutoa uamuzi wa rufaa tano za kupinga kuharamishwa kwa mchakato wa BBI.

Rais wa mahakama ya Rufaa Daniel Musinga ambaye ameongoza kikao cha kuamua mwelekeo wa kesi hiyo amesema rufaa hizo tano kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta, kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga, mwanasheria mkuu Paul Kihara Kariuki, tume ya uchaguzi na mipaka IEBC na jopokazi la BBI zitasikilizwa kwa pamoja.

Musinga amesema kesi hiyo itasikilizwa kuanzia tarehe 29 mwezi huu wa Juni hadi tarehe mbili mwezi ujao wa Julai kwa kuzingatia masharti ya kuzuia msambao wa corona.

Baadhi ya mawakili kwenye kesi hiyo pia wataruhusiwa kuhudhuria vikao hivyo kwa njia ya mtandao, haswa wale walio hatarini kuambukizwa virusi vya corona huku vyombo vya habari vikiruhusiwa kupeperusha vikao hivyo moja kwa moja.

Wakati uo huo

Tume ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC imepata afueni ya muda baada ya kuruhusiwa kuendelea na majukumu yake had pale rufaa waliyowasilisha mahakamani itakaposkizwa na kuamuliwa.

Hata hivyo Jaji Daniel Musinga amezuia tume hiyo dhidi ya kuendelea mbele na mpango ya kuandaa kura ya maamuzi kupigia kura mswada wa BBI hadi pale rufaa hiyo itaskilizwa na uamuzi kutolewa.

Tume hiyo ilielekea mahakamani kupinga uamuzi wa mahakama kuu kwamba kikatiba, makamishna watano hawatoshi kuendesha shughuli za tume hiyo.