Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye amewasili humu nchini kwa ziara rasmi ya siku mbili.
Ndege iliyombeba Rais huyo na ujumbe wake imetua katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Kisumu kabla ya kufululiza hadi katika ikulu ndogo ya Rais Kisumu ambapo amepokelewa na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta.
Rais Ndayishimiye ameandaliwa waride la heshima na wanajeshi wa Kenya ambao pia wamepiga mizinga ishirini na moja kwa heshima ya Rais huyo.
Kwa sasa, marais hao wawili wanafanya mazungumzo ya faragha kabla yao kuandamana kuzindua miradi kadhaa ya maendeleo katika eneo la Nyanza.
Ndayishimiye atakuwa mgeni wa heshima kwenye maadhimisho ya sikukuu ya madaraka hapo kesho mjini Kisumu.
Katibu katika wizara ya usalama wa ndani Dr Karanja Kibicho amesema maandalizi yote yamekamilika kabla ya maadhimisho hayo ya kesho katika uwanja wa michezo wa Jomo Kenyatta kaunti ya Kisumu.
Wakenya huadhimisha siku ya Madaraka kukumbuka siku ambayo Kenya ilipata uhuru wa kujitawala mwaka 1963.