Rais Uhuru Kenyatta kwa mara nyingine amesisitiza kwamba ushirikiano wake na aliyekuwa kiongozi wa upinzani Raila Odinga ni kuhakikisha kwamba wanatimiza ndoto za waanzilishi wa nchi hii za kuwa na taifa lenye umoja na mshikamano wa kitaifa.

Akizungumza baada ya kukutana na wabunge kutoka eneo la Nyanza kabla ya ziara yake mjini Kisumu wiki ijayo, rais amesema makusudi yao ni kuhakikisha kwamba vijana wamepata kazi na wana uwezo kupata mahitaji muhimu sawa na taifa ambalo kila Mkenya anajivunia.

Na huku kukiwa na hofu kuhusu msambao wa virusi vya corona katika kaunti ya Kisumu kabla ya maadhimisho ya Madaraka Dei, waziri wa afya Mutahi Kagwe amesema mikakati kabambe imewekwa kudhibiti msambao wa ugonjwa huo wakati wa maadhimisho hayo.

Mbunge wa Seme Dr. James Nyikal ametaja kuwa uwanja ambapo sherehe hizo zitaandaliwa una uwezo wa kubeba watu elfu thelathini na tatu ila ni watu elfu tatu peke yake ambao wataruhusiwa.

Rais Kenyatta ameratibiwa kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo wakati wa ziara hiyo katika eneo la Nyanza.