Baadhi ya viongozi wa eneo la mlima Kenya wamefanya mkutano wa mashauriano kuamua mustakabali wa eneo hilo kisiasa.

Wakiongozwa na gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui, viongozi hao wakiwemo magavana na wabunge wamesema mkutano huo ni mwanzo tu wa misururu ya mikutano ili kujadili kwa kina jinsi ya kuwaleta pamoja watu wa mlima Kenya kuzungumza kwa sauti moja kabla ya uchaguzi wa 2022.

Magavana Ann Waiguru wa Kirinyaga na Mutahi Kahiga wa Nyeri waliohudhuria mkutano huo pia wamesema nia yao ni kuhakikisha kuwa mahitaji ya watu wa eneo hilo yanawakilishwa vyema serikalini.

Gavana Mwangi wa Iria wa Murang’a, aliyekuwa gavana wa Kiambu William Kabogo na aliyekuwa mbunge wa Dagoretti Kusini Dennis Waweru pia wamehudhuria mkutano huo.

Mkutano huo unajiri siku chache baada ya spika wa bunge la kitaifa Justin Muturi kutawazwa kama msemaji wa mlima Kenya zoezi ambalo limewagawanya viongozi wa eneo hilo.