Meneja wa mawasiliano wa tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC Tabitha Mutemi na aliyekuwa naibu mwenyekiti wa tume ya ardhi nchini NCL Abigael Mbagaya ni miongoni mwa watu 669 waliotuma maombi kujaza nafasi za makamishna wanne wa IEBC.

Mutemi ameorodheshwa siku chache baada ya wabunge kumtetea dhidi ya kuondolewa kama mwanachama wa bodi ya baraza la vyombo vya habari nchini MCK.

Wengine waliotuma maombi yao kujaza nafasi hizo za makamishna wa IEBC ni mawakili Alice Yano aliyehojiwa kwa wadhifa wa Jaji Mkuu na jaji wa mahakama ya upeo, Harriette Chiggai na Norman Magaya.

Jopo linaloongoza mchakato wa kuwatafuta makamishna wapya wa IEBC chini ya uenyekiti wake Elizabeth Muli lilipokea maombi kutoka kwa watu 700 ila ikawachuja wengine kwa kukosa kuafikia vigezo vilivyowekwa.

Rais Uhuru Kenyatta aliteua jopo hilo kufuatia kujiuzulu kwa waliokuwa makamishna Roselyn Akombe, Paul Kurgat, Margaret Mwachanya na Connie Maina.