Washukiwa wa ulaghai akiwemo afisa mkuu katika idara ya magereza ambao wamewatapeli wakenya wanaotafuta kazi mamilion ya pesa wanatazamiwa kufikishwa mahakamani hii leo.

Washukiwa wawili kati ya genge la matapeli hao walikamatwa mwishoni mwa wiki iliyopita huku mshukiwa mkuu Grace Nyamohanga almaarufu Nasra ambaye ni sajenti mkuu katika gereza la akina mama la Langata akijisalimisha kwa maafisa wa idara ya upelelezi DCI jana jioni.

Katika taarifa, DCI inasema genge hilo ambalo linawajumuisha maafisa wengine wa magereza limewalaghai wakenya zaidi ya shilingi million ishirini baada ya kuwahadaa kuwa wangepata kazi katika idara mbalimbali za serikali ikiwemo mamlaka ya bandari nchini KPA, idara ya jeshi KDF, idara ya ujasusi NIS miongoni mwa zingine.

Kwa mfano DCI inasema mama mmoja kutoka kaunti ya Kiambu alilipa shilingi elfu mia nane baada ya kuhadaiwa kuwa watoto wake watatu wangepata kazi katika idara mbalimbali za serikali.

Hata hivyo mama huyo alikimbilia majasusi wa DCI baada ya kugundua kuwa barua alizopewa kwa watoto wake kuripoti kazini zilikuwa ghushi.

Januari mwaka huu, DCI inasema kuwa vijana sitini waliokuwa wakitafuta kazi walilipa wakora hao kati shilingi elfu mia tatu na elfu mia nne kila mmoja baada ya kuhadaiwa kuwa wangepewa kazi katika mamlaka ya bandari nchini KPA.

Badala yake, washukiwa hao walipelekwa ziara katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta na kisha kuandaliwa mlo mzuri katika mkahawa wa kifahari na kutakiwa kurejea nyumbani kusubiri tarehe ya kuripoti kazini, tarehe ambayo hadi kufikia sasa imesalia ndoto.