Mahakama imewakubalia Polisi kumzuilia mtu, mkewe na mvulana wao kwa siku tatu zaidi kwa tuhuma za kumuua binti yao katika eneo la Jamhuri jijini Nairobi.

Mahakama imeridhia ombi la Polisi kuendelea kuwazuilia watatu hao walioshikwa Jumamosi iliyopita ili kuwapa muda wa kutosha kukamilisha uchunguzi.

Watatu hao Frankline Ntwiga, mkewe Benedetta Mbeni na mtoto wao wa kiume Ian Marangu Ntwiga wanatuhumiwa kumuua mwanafunzi huyo wa shule ya wasichana ya Kiteta kaunti ya Makueni kwa madai ya kutoroka nyumbani.

Idara ya upelelezi nchini DCI inaarifu kuwa baba mtoto huyo alimpelaka katika hospitali ya Coptic usiku wa Alhamisi wiki iliyopita kufanyiwa ukaguzi wa kimatibabu ambao ulionyesha alikuwa mzima.

Hata hivyo walipofika nyumbani, watatu hao walimwangukia kwa kichapo kutumia kipande cha mfereji na walipoona amezirai wakamkimbiza tena katika hospitali hiyo ila alikuwa tayari ashakata roho.

Madaktari wanasema mwili wa msichana huyo ulikuwa na majeraha kila mahali ishara kuwa alikuwa amedhulumiwa.