Mwanamke wa miaka 25 katika kaunti ya Kisii anatazamiwa kufikishwa mahakamani hii leo kwa tuhuma za kumuua mtoto wake wa miaka tisa kwa kupoteza shilingi kumi alizotakiwa kununua chapati.

Grace Nyandusi anadaiwa kutekeleza mauaji hayo Jumamosi jioni baada ya kumgonga mwanawe na kifaa butu kichwani.

Naibu chifu wa eneo hilo Calvin Kengara amesema mwanafunzi huyo wa shule ya msingi ya Gesare eneobunge la Nyaribari Chache alitumwa kununua chapatti na mamake lakini akapoteza shilingi kumi alizopewa ndani ya shamba la miwa alipopitia.

Aliporudi kumweleza mamake kilichotokea, mshukiwa anadaiwa kupandwa na mori kabla ya kuchukua kifaa butu na kumgonga kichwani.

Alipoona mwanawe amezirai, alianza kupiga kamsa kuomba usaidizi wa majirani, lakini tayari mtoto alikuwa amefariki.