Chama tawala cha Jubilee kimeamua kuwahoji watu wakaopeperusha bendera yake kwenye chaguzi ndogo za Kiambaa na wadi ya Muguga badala ya kufanya uchaguzi wa mchujo.

Wanaotaka kuwania chaguzi hizo kwa tiketi ya Jubilee wametakiwa kufika katika makao makuu ya chama hicho kuhojiwa kesho Jumamosi.

Katibu mkuu wa chama hicho Raphael Tuju amesema watakaofaulu watapewa cheti kuambatana na katiba ya chama.

Jubilee imebadilisha mbinu baada ya kutoka mikono mitupu kwenye chaguzi ndogo za Juja, Rurii na Bonchari.

Wapiga kura katika wadi wa Muguga watarudi debeni Julai 15 kumchagua MCA mpya kufuatia kifo cha Eliud Ngugi huku eneo bunge la Kiambaa likimtafuta mbunge mpya kufuatia kufariki kwa Paul Koinange.