Makachero wa idara ya upelelezi DCI wamemuokoa pasta John Chege wa kanisa la Kianglikana la Kabete kutoka kwa majambazi waliokuwa wamemteka nyara.

Muhubiri huyo alitekwa nyara mwendo wa saa mbili jana usiku na genge la watu wanne alipokuwa anaelekea nyumbani kwake.

Inaarifiwa kwamba majambazi hao walichukua usukani wa gari lake na kulielekeza Kiamumbi kaunti ya Kiambu.

Polisi walipoambiwa, walianza kufuata gari hilo na kisha kulipata katika eneo la Jacaranda.

Majambazi hao walipoagizwa kujisalimisha, walikaidi amri hiyo na kisha kukatokea tukio la ufyatulianaji wa risasi ambapo washukiwa wawili waliuawa.

Washukiwa wengine wawili walifaulu kutoroka wakiwa na majeraha huku maafisa hao wakifaulu kumuokoa pasta Chege.