Kampeni ya chanjo dhidi ya polio kwa watoto walio chini ya umri wa miaka tano itazinduiwa Ijumaa hii katika Kaunti ya Garissa

Wizara ya Afya imesema inalenga kutoa chanjo kwa watoto milioni 3.4 wakati wa kampeni hiyo na kuondoa wasiwasi kuhusiana na usalama wake kwani tayari imepitia taratibu zote za usalama.

Katika taarifa yake iliyosomwa na Mkuu wa afya ya Umma Dr. Franci Kuria, Waziri wa afya Mutahi Kagwe amesema ni haki ya kila mtoto chini ya umri ya miaka mitano kupata chanjo wakati wa kampeni hiyo itakayoendelea hadi jumatano wiki ijayo.

Haya yanajiri wakati visa sita vya ugonjwa huo vikiripotiwa katika Kaunti ya Garissa na Mombasa, hali ambayo imezua wasiwasi wa kuwepo kwa mrupuko wa polio nchini

Zoezi la kutoa chanjo hiyo litaendeshwa katika kaunti za Mandera, Isiolo, Wajir, Garissa, Lamu, Tana River, Kilifi, Mombasa, Kitui, Machakos, Kajiado, Kiambu na Nairobi.

Wazazi na walezi ambao watakosa kuwapeleka watoto wao walio chini ya miaka mitano kupata chanjo hiyo ya polio wameonywa kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.