Pavel Oimeke wa chama cha ODM ameibuka mshindi wa uchaguzi mdogo katika eneobunge la Bonchari kaunti ya Kisii uliofanyika jana.

Oimeke amepata kura 8, 049 na kumshinda Zebedeo Opore wa Jubilee aliyeibuka wa pili baada ya kupata kura 7,279.

Mjane wa aliyekuwa mbunge wa sehemu hiyo marahemu John Oroo Oyioka, Teresa Bitutu aliyepeprusha bendera ya chama cha UDA ambacho kinahusihwa na naibu Rais William Ruto ameridhika katika nafasi ya tatu na kura 6,964.

Oimeke ambaye ni mkurugenzi wa zamani wa tume ya kudhibiti kawi nchini EPRA sasa atasubiri kuapishwa ili kuwawakilisha wananchi wa Bonchari hadi uchaguzi mkuu wa Agosti mwakani.

Chama cha ODM kimekaribisha ushindi huo licha ya kulalama kuwa chama tawala kilitumia maafisa wa usalama kuwakandamiza na kudai kuwa madiwani wake kadhaa na maafisa wengine walikamatwa wakati wa zoezi hilo.