Muwaniaji wa chama cha Jubilee katika uchaguzi mdogo wa eneobunge la Juja Susan Njeri Waititu sasa anadai kura hizo zimeibiwa.

Akiandamana na viongozi kadhaa wa Jubilee kaunti ya Kiambu akiwemo mbunge Jude Njomo na wafuasi wake, Njeri ambaye ni mjane wa aliyekuwa mbunge wa sehemu hiyo marahemu Francis Waititu ametaka kura hizo kuhesabiwa tena.

Njeri ameondoka kwenye kituo cha kuhesabu kura cha Mangu kulalamikia matokeo hayo anayosema hayaonyeshi picha halisi ya kile kilichofanyika.

AWALI

Tume ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC ilirejelea zoezi la kuhesabu kura katika uchaguzi mdogo wa Juja kaunti ya Kiambu baada ya utulivu kurejelewa.

Mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati ametoa hakikisho kuwa kura zilizopigwa zimelindwa na kwamba hakuna udanganyifu umeshuhudiwa.

Chebukati amesema watamwandikia mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma kuwafungulia mashtaka viongozi waliovuruga zoezi hilo.

Afisa mkuu wa uchaguzi katika eneobunge hilo Justus Mbithi amesema watatangaza matokeo ya uchaguzi huo kufikia saa nane mchana hii leo.

Tume hiyo inamshtumu gavana wa Kiambu James Nyoro kwa kuongoza kundi la wahuni kuvuruga zoezi hilo.