Muungano wa mashirika yasiyo ya kiserikali umewarai watetezi wa marekebisho ya katiba kupitia BBI wasivunjwe moyo ya uamuzi wa mahakama uliosimamisha mchakato huo.

Kupitia kwa mwenyekiti wao Suba Churchill, mashirika hayo yanahoji kuwa marekebisho hayo ya katiba yana umuhimu mkubwa kwa taifa la Kenya na wanafaa kuendelea mbele licha ya kutiwa breki na mahakama kuu.

Kwa mfano, mashirika hayo yanahoji kuwa BBI ina mapendekezo mazuri yatakayolisaidia taifa kutatua hali ya vuta nikuvute kila baada ya uchaguzi na migawanyiko inayosababishwa na upinzani wa kisiasa wakati wa uchaguzi.

Hayo yakijiri

Serikali Jumatatu inatazamiwa kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama kuu uliosimamisha ubadilishaji wa katiba kupitia mchakato wa BBI.

Mwanasheria mkuu Kihara Kariuki ameifahamisha mahakama kupitia kwa notisi kwamba hawakuridhishwa na uamuzi huo wa jopo la majaji watano; Joel Ngugi, George Odunga, Jairus Ngaah, Teresia Matheka na Chacha Mwita.

Majaji hao waliamuru kwamba mchakato huo unakiuka katiba na kwamba rais hana mamlaka ya kuanzisha ubadilishaji wa katiba na badala yake kuhoji kuwa ni mkenya wa kawaida ndiye aliye na uwezo huo.

Majaji hao waliamuru kwamba tume ya uchaguzi na mipaka IEBC haijabuniwa kisheria kusimamia kura ya maamuzi na kwamba Wakenya hawakuhusishwa kikamilifu kupitia kutolewa kwa elimu kwa umma kuhusu BBI.