Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini (IEBC) imesema itakata rufaa wiki hii dhidi ya uamuzi wa mahakama kuu ulioamuru kwamba haina makamishna wa kutosha kuwajibukia majukumu yake.

Mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati akizungumza siku moja kabla ya kuandaliwa kwa uchaguzi mdogo katika maeneo bunge ya Juja na Bonchari amesema uamuzi huo unakinzana na ule uliotolewa awali kwamba makamishna watatu wako na uwezo wa kuendesha majukumu ya tume hiyo ipasavyo.

Chebukati ameeleza kwamba mkinzano huo kwenye maamuzi ya mahakama kuu ndio sababu kuu itakayowafanya kutafuta ufafanuzi wa mahakama ya rufaa ili kujua mwelekeo utakaofuatwa.

Kuhusu uchaguzi huo mdogo, Chebukati amesema kila kitu kii shwari na wanatarajia kusimamia uchaguzi kwa njia huru na wazi.