Seneta mteule Isaac Mwaura amepata afueni ya muda baada ya mahakama kuzuia kufurushwa kwake na chama cha Jubilee hadi kesi aliyowasilisha mahakama itakaposikilizwa na kuamuliwa.

Jaji wa mahakama kuu Joseph Sergon ameratibu kesi hiyo kusikilizwa Mei 24.

Uamuzi huu wa mahakama unajiri saa chache baada ya spika wa bunge la Senate Ken Lusaka kutangaza kiti cha Mwaura kuwa wazi kupitia kwa gazeti rasmi la serikali kuanzia Mei 7 mwaka huu wa 2021.

Maseneta wakiongozwa na James Orengo wamemtetea Mwaura wakitaka uamuzi wa kumfurusha kubatilishwa.

Mwaura alipoteza kiti chake baada ya jopo la kutatua mizozo ya vyama vya kisiasa kuamuru kwamba chama chake cha Jubilee kilikuwa sawa kumfurusha kwa kuzingatia sheria za vyama vya kisiasa.

Jubilee ilimtimua Mwaura kwa misingi kwamba amekuwa akiuza sera za chama kingine kinyume na kanuni zinazolinda vyama vya kisiasa.