Seneta wa Nyamira Okong’o Omogeni ataongoza kamati ya watu 11 itakayochunguza kung’olewa kwa gavana wa Wajir Mohammed Mohamud Abdi.

Wanachama wa kamati hiyo waliamua kwa kauli moja kumchagua Omogeni kuwaongoza muda mfupi baada ya bunge la Senate kupiga kura kuunga mkono hatma ya gavana huyo kubainiwa na kamati maalum.

Naibu mwenyekiti wa kamati hiyo atakuwa seneta wa Nakuru Susan Kihika.

Maseneta wengine kwenye kamati hiyo ni; Sakaja Johnson (Nairobi), Mwangi Githiomi (Nyandarua), Hargura Godana (Marsabit), Fredrick Outa (Kisumu), Agnes Muthama (Machakos), Issa Juma (Kwale), Mithika Linturi (Meru) na maseneta wateule Christine Zawadi na Petronilla Were.

Gavana huyo anatuhumiwa kwa makosa mbalimbali ikiwemo utumizi mbaya wa mamlaka na ufisadi, ukiukaji wa haki za ununuzi, kukosa kuelezea matumizi ya pesa za kaunti, kukosa uwajibikaji miongoni mwa mengine.

Itakumbukwa kwamba madiwani 37 mnamo Aprili 27 mwaka huu walipiga kura kuunga mkono hoja hiyo huku 10 wakipiga kura ya kupinga.