Chama cha ODM kimemuondoa mbunge wa Rarieda Otiende Amollo  kwenye kamati muhimu ya bunge la kitaifa kuhusu haki na maswala ya kisheria (JLAC).

Nafasi ya Amollo ambaye alikuwa naibu mwenyekiti kwenye kamati hiyo inatwaliwa na mwenzake wa Ruaraka TJ Kajwang.

Mabadiliko hayo yanatazamiwa kudhibitishwa rasmi Jumatano wakati wa vikao vya alasiri.

Kung’olewa kwa Otiende Amollo kwenye kamati hiyo kunadaiwa kuchochewa na tofauti zilizoibuka katika chama cha ODM kinachoongozwa na Raila Odinga kuhusu mswada wa marekebisho ya katiba BBI.

Hatma ya seneta wa Siaya James Orengo vile vile iko kwenye mizani ikiarifiwa kwamba naye pia alichukua msimamo sawa na ule wa Amollo na wendani wa Raila wanawataja kama wasaliti chamani.

Hayo yakijiri

Bunge halina jukumu la kufanyia marekebisho mswada wa kubadilisha katiba kupitia mchakato wa BBI licha ya shinikizo kutoka kwa baadhi ya wabunge.

Akitoa uamuzi wakati kikao maalum cha bunge kujadili mswada huo, spika wa bunge la kitaifa Justine Muturi ameamuru kwamba bunge halina jukumu la kuurekebisha mswada huo kwa sababu umetoka kwa wananchi.