Walimu ambao wanasahihisha mtihani wa kidato cha nne KCSE katika shule ya wasichana ya State House wameshiriki mgomo kulalamikia kutopewa marupurupu yao.
Walimu hao wanasema juhudi zao kutafuta suluhu kutoka kwa wizara ya elimu zimegonga mwamba hali ambayo imewalazimu kushiriki mgomo.
Kando na marupurupu, walimu hao wanataka kuongezwa kwa idadi ya vituo vya kusahihishia ili kuzingatia sheria za wizara ya afya za kupambana na virusi vya korona.
Walimu hao pia wanadai serikali iliahidi kuwalipa wiki kadha zilizopita na hadi sasa hilo limebakia kuwa ni msemo tu bila vitendo.
Hapo awali katibu mkuu wa chama cha walimu wa sekondari (KUPPET) Akelo Misori aliashiria hali ya atiati iwapo serikali itakosa kuafikia makubaliano na kuwalipa walimu hao.