Rais wa Tanzania Samia Suluhu anayetazamiwa kuwasili humu nchini baadaye hii leo kwa ziara rasmi ya siku mbili, atahutubia kikao cha pamoja cha wabunge na maseneta hapo kesho.

Katika notisi, maspika Justin Muturi wa bunge la kitaifa na Ken Lusaka wa seneti, wamewataka wabunge na maseneta kufika bungeni hapo kesho saa nane unusu mchana kwa vikao hivyo.

Ziara ya Rais Samia nchini inatazamiwa kuboresha uhusiano baina ya mataifa haya mawili.

Rais Samia atapokelewa na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta katika ikulu ya Rais, Nairobi, kabla ya kukagua gwaride la heshima kutoka kwa majeshi ya Kenya ambayo pia yatapiga mizinga ishirini na moja kama ishara ya heshima.

Wawili hao kisha watafanya mazungumzo ambayo yatajikita katika kuimarisha biashara baina ya mataifa hayo huku Rais Samia akiratibiwa kuhutubia mkutano wa jukwaa la wafanyibiashara wa Kenya na Tanzania.