Waziri wa usalama Dkt. Fred Matiang’i amesema kanuni mpya za Polisi zitaletwa ili kuwapiga marufuku maafisa wa Polisi kuoana kuhakikisha kuwa nidhamu inadumishwa.

Akizungumza alipoongoza uzinduzi wa hafla ya kutoa mafunzo kwa wakuu wa Polisi katika taasisi ya Kiganjo, kaunti ya Nyeri, waziri Matiang’i anahoji kwamba hatua hii ni katika juhudi za kuzuia maafa yanayotokea miongoni mwa Polisi ambao hujiua na kisha kuwageukia wapenzi wao.

Tume ya huduma za Polisi (NPS) inatazamiwa kuleta mabadiliko hayo kufikia mwezi Julai mwaka huu wa 2021.

Wakati uo huo, Dkt. Matiang’i anasema watakapofuzu, wakuu hao wa Polisi watasaidia katika kuimarisha usalama, huku akihoji kuwa suala la kudumisha usalama si tena matumizi ya nguvu au mtutu wa bunduki.

Matiang’i amewataka makadeti hao kushirikiana na jamii watakapofuzu ikiwemo viongozi wa kidini na kisiasa ili kufanikisha usalama wa taifa.