Kambi za wakimbizi za Dadaab na Kakuma zitafungwa kufikia mwishoni mwa mwezi Juni mwaka ujao 2022 imetangaza serikali ya Kenya.
Wizara ya usalama wa ndani imeliarifu shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi duniani UNHCR kwamba kambi hizo zitafungwa Juni, 30 mwaka ujao huku ikitangaza taratibu zitakazotumika kufunga kambi hizo zinazotoa hifadhi kwa zaidi ya wakimbizi laki tano.
Mikakati hiyo ni pamoja na kuwarejesha makwao kwa hiari wakimbizi watakaokuwa tayari kufanya hivyo na pia kuwaruhusu baadhi kuchangamana na jamii ya Kenya.
Shirika la Amnesty International kupitia mkurugenzi wake mkuu tawi la Kenya Irungu Houghton limekaribisha taratibu hizo likisema serikali ya Kenya imetoa muda wa kutosha kuhakikisha kuwa utu umezingatiwa wakati wa shughuli nzima ya kufunga kambi hizo.