Kuanzia Jumamosi, hakutakuwa na ndege zinazotoka wala kuingia India huku Kenya ikitangaza marufuku ya siku 14 kufuatia kuongezeka kwa maambukizi ya corona nchini humo.

Waziri wa afya Mutahi Kagwe ameagiza kuwa wasafiri kutoka nchini humo lazima wajiweke kwenya karantini ya wiki mbili kwa gharama yao.

Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa idadi ya waliofariki kutokana na virusi vya corona nchini India imepindukia watu laki mbili.

Hii ni baada ya zaidi ya watu elfu tatu wengine kufariki katika kipindi cha saa ishirini na nne zilizopita hiyo ikiwa ni rekodi ya vifo kwa siku moja.

Kwa sasa India imesajili visa milioni 18 vya maambukizi na katika masaa ishirini na nne yaliyopita watu 360,000 wameambukizwa virusi vya corona.