Malumbano makali yameshuhudiwa katika bunge la kitaifa wakati wa kujadili na kisha kufutilia mbali ripoti inayopendekeza kuondolewa kwa Tabitha Mutemi kama mwanachama wa bodi ya baraza la vyombo vya habari (MCK).

Kamati ya bunge la kitaifa kuhusu habari na mawasiliano chini ya uenyekiti wake mbunge wa Marakwet Magharibi William Kipsang’ ilipendekeza kung’olewa kwa Mutemi kwa misingi kwamba Mutemi hawezi hudumu kwenye bodi hiyo ilhali yeye bado ni mfanyikazi wa tume ya uchaguzi IEBC.

Hata hivyo baadhi ya wabunge wakiongozwa na David Sankok walifutilia mbali mapendekezo ya ripoti hiyo wakitaja kama ya maonevu dhidi ya Tabitha Mutemi.

Awali, tume IEBC kupitia kwa mwenyekiti wake Wafula Chebukati ilitishia kumchukulia Mutemi hatua za kisheria kwa kukiuka mkataba wake wa kazi ambapo alikubali kuchukua kazi nyingine wakati bado alikuwa mfanyikazi wake.