Mvutano wa uongozi katika chama cha mawakili nchini LSK umeishia kwa makundi hasimu kuteua majina mawili tofauti kuwakilisha chama hicho kwenye jopo litakaloongoza mchakato wa kuwatafuta makamishna wanne wa tume ya uchaguzi IEBC.

Kundi moja limemteua wakili Dorothy Jemator kuwa katika jopo hilo ilhali kundi lingine likiongozwa na rais wa LSK Nelson Havi likimpendekeza Morris Kimuli kuwa kwenye jopo hilo.

Hata hivyo afisa mkuu mtendaji wa chama hicho Mercy Wambua amepuuzilia mbali uteuzi wa Havi na wenzake akisema unakiuka kanuni za chama hicho.

Majina ya watakaokuwa kwenye jopo yanatazamiwa kukabidhiwa rais kuanza mchakato wa kujaza nafasi hizo za IEBC.

Jopo hilo linafaa kuwa na wanaume na wanawake wawili kutoka PSC, mwakilishi wa LSK na wawakilishi wawili wa makundi ya kidini.

Hatua hii inakuja baada ya rais Kenyatta kutangaza wazi nafasi za makamishna wanne waliojiuzulu baadhi yao wakizawadiwa kazi za serikali.

Nafasi hizo zilisalia wazi kufuatia kujiuzulu kwa makamishna Consolata Nkatha, Paul Kurgat, Roselyne Akombe na Margaret Mwachanya.