Mahakama ya Marekani imemkuta na hatia afisa wa polisi wa zamani kufuatia kifo cha Mmarekani mweusi George Floyd mwaka jana.

Derek Chauvin, 45, alinaswa kwenye video akipiga goti kwenye shingo la marehemu Floyd kwa zaidi ya dakika tisa alipokamatwa mwezi Mei mwaka uliopita.

Video hiyo iliyotazamwa sana iliibua hisia kali na kusababisha maaandamano dhidi ya ubaguzi wa rangi kote duniani na utumiaji wa nguvu kupita kiasi unaofanywa na kikosi cha polisi.

Chauvin alipatikana na makosa matatu: mauaji ya kiwango cha pili, kiwango cha tatu na mauaji bila kukusudia.

Polisi huyo atabaki kizuizini hadi atakapohukumiwa na huenda akafungwa jela kwa miaka nyingi.

Uamuzi huo umesababisha umepokelewa kwa shangwe huku maelfu ya Marekani wakiendelea kushangilia hukumu hiyo ya kwanza katika historia ya taifa hilo.

Rais Joe Biden amesema kutiwa hatiani kwa Derek Chauvin kwa mauaji ya George Floyd kunaweza kuwa hatua kubwa katika vita dhidi ya ubaguzi wa kimfumo, lakini hakutoshi.