Rais wa sasa wa mahakama ya Rufaa William Ouko kwa sasa amehojiwa na tume ya huduma za mahakama (JSC) kwa wadhifa wa Jaji Mkuu.

Jaji Ouko ameiambia JSC kwamba uamuzi kamili wa kesi za kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu unafaa kutolewa chini ya siku tisini kulingana na katiba ili kuhakikisha upatikanaji wa haki.

Aidha jaji Ouko ametetea mahakama ya leba na ardhi dhidi ya kuchelewa kusikiliza na kuamua kesi akisema kunatokana na changamoto ya kutokuwa na majaji wa kutosha katika idara ya mahakama.

Hata hivyo Ouko anasema kuna haja ya idara ya mahakama kulainisha  mawasiliano ili kuafikia malengo yake.

Ouko ameongeza licha ya kuwepo kwa mikakati ya kuleta mabadiliko katika idara ya mahakama, kiwango cha fedha kinachotengewa idara hiyo ni cha chini na hivyo kulemaza utekelezwaji wa mipango hiyo.

Ouko ni mzaliwa wa mwaka 1961 katika kaunti ya Siaya na aliidhinishwa kuwa wakili mwaka 1987.

Wengine waliohojiwa kwa wadhifa huo ni pamoja na mawakili Fred Ngatia na Philip Murgor, majaji David Marete, Martha Koome, Juma Chitembwe na msomi wa maswala ya kisheria Profesa Kameri Mbote.