Baraza kuu la vyombo vya habari nchini (MCK) limeikosoa idara ya upelekezi (DCI) kufuatia msimamo wake kuhusu taarifa ya upekuzi iliyopeperushwa na Citizen TV kuhusu namna majambazi wanavyokomboa silaha kutoka kwa maafisa wa Polisi kutekeleza uhalifu.

MCK kupitia taarifa imesema hatua ya mkurugenzi wa DCI George Kinoti kukashifu makala hayo ya Purity Mwambia inahujumu uhuru wa kujieleza na kutaarifu umma kuhusu yanayowahusu.

Taarifa ya baraza hilo inakuja saa chache baada ya Kinoti kuita mkutano na waandishi wa habari ambapo alikana madai ya Polisi kuwakodisha wahalifu bunduki akisema hawakupewa nafasi ya kujitetea kwenye makala hayo.

Kulingana na idara hiyo bunduki zinazodaiwa kununuliwa kutoka kwa polisi, zimetengenezwa kutoka Uchina na hazina nambari kamuli za usajili na hivyo havitumiki na polisi.

Makala hayo yaliyopeperushwa Jumapili iliyopita yalifichua namna Polisi wanadaiwa kuendesha uhalifu kwa kukodisha sare, pingu na bunduki zao kwa wahalifu kwa shilingi elfu moja pekee.