Idadi kubwa ya wakenya wanategemea mikopo kununua vyakula na sasa wana madeni ambayo yanawalemea kulipa.

Utafiti uliotolewa na shirika la kitaifa la takwimu unaonyesha kuwa asilimia 51 ya wakenya wamekuwa wakikopa ili kuweka chakula mezani.

Utafiti huo pia umeonyesha kuwa asilimia 44 ya wakenya wamepunguza idadi ya mlo kwa siku, wengi pia wakipunguza kiasi cha chakula wanachotumia kutokana na makali ya janga la corona.

Utafiti uo uliotolewa kwenye ripoti kuhusu hali ya vyakula nchini unaonyesha kuwa asilimia 33 wakenya wanategemea chakula kutoka cha msaada kutoka kwa wahisani.

Asilimia nyingine ishirini na moja ya wakenya waliohojiwa wanasema walikazia watu wazima kula ili watoto wapate chakula huku asilimia 16 wakishinda siku nzima bila kula, mradi watoto wapate chakula.

Utafiti huo ulifanywa kati ya tarehe mbili na tarehe kumi na moja mwezi Mei na kati ya tarehe thelathini Mei na tarehe sita juni mwaka uliopita.

Watu 15,840 walihojiwa kwenye awamu ya kwanza na wengine 14,616 kuhojiwa kwenye awamu ya pili.