Aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga ameelezea kusikitishwa kwake na kuongezeka kwa visa vya dhulma za kijinsia ambavyo vinaishia kusababisha maafa.

Katika taarifa, Odinga amesema kuna haja kama taifa kuwa na mjadala kuhusu dhulma za kijinsia katika juhudi za kuzuia ongezeko la mauaji katika familia.

Odinga ambaye pia ni kiongozi wa chama cha ODM amesema inasikitisha mtu kumuaa mwenzake aliyeahidi kumpenda na kumdhamini.

Odinga anawasihi wapenzi kuondoka kwenya mahusiano iwapo hawawezi kusuluhisha tofauti baina yao badala ya kugeukiana na kusababisha maafa.

Haya yanajiri siku moja tu baada ya Evans Karani, mshukiwa wa mauaji ya mpenziwe Catherine Nyokabi kuwaambia Polisi kwamba hajutii unyama aliofanya na kuomba mahakama kuharakisha hukumu dhidi yake.