Huku taifa la Kenya likiendelea kushuhudia upungufu wa dawa za kupunguza makali ya ugonjwa UKIMWI, ARVs, shirika la kutetea haki za kibinadamu la Amnesty International limeelezea wasiwasi kuhusu hali hiyo.
Shirika hilo kupitia meneja wake wa kampeini Diana Gichengo linaonya kwamba upungufu huo ambao umeshuhudiwa kwa muda sasa unahatarisha maisha ya wagonjwa milioni moja nukta tano ambao wamenyimwa fursa ya kupata msaada huo muhimu wa kiafya.
Na ili kukabiliana na changamoto hii, Amnesty International inaitaka wizara ya afya kushughulikia tatizo hilo haraka upesi na kutangaza wazi hatua zinazochukuliwa kuhakikisha uwajibikaji katika shirika la kununua na kusambaza vifaa vya matibabu KEMSA.
Shirika hilo vile vile linalitaka bunge kuwaambia Wakenya ukweli kuhusu uchunguzi waliofanya kuhusu maswala mbalimbali yanayoambatana na afya.
Itakumbukwa kwamba mzigo wenye dawa hizo umekwama katika bandari ya Mombasa kwa miezi kadhaa sasa kufuatia mvutano baina ya serikali ya Kenya na wafadhili wa shirika la USAID kuhusu ushuru.