Watahiniwa wa mtihani wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE) mwaka 2020 walijikakamua na kufanya vyema licha ya hali ngumu iliyosababishwa na janga la kimataifa la corona.

Waziri wa elimu Profesa George Magoha anasema licha ya wengi kuwa na wasiwasi kuwa wanafunzi hao watakosa kufanya vyema katika mtihani huo, matokeo yameonyesha kutokuwepo kwa mabadiliko yoyote ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Kwenye matokeo hayo, Faith Mumo wa shule ya Karimwailu iliyoko Makueni alitangazwa mwanafunzi bora kwa kupata alama 433 huku Wesonga Nanzala wa shule ya Wasichana ya Chogoria na Muriithi Gakenia wa shule ya wasichana ya Maseno wakiibuka wa pili kwa kupata alama 432.

Kwa mujibu wa Profesa Magoha, shule za umma kwa mara nyingine zimefanya vyema ikilinganishwa na shule za kibinafsi kwenye mtihani huo.

Aidha, waziri Magoha amesema wanafunzi wa kike wameongoza kwa kufanya vyema katika masomo ya Kiingereza, Kiswahili na somo la ishara ikilinganishwa na wenzao wa kiume ambao wameongoza katika masomo ya Hesabu, Sayansi na somo la kijamii na dini.