Kamati ya pamoja iliyobuniwa kutatua mzozo wa vikwazo vya usafiri baina ya Kenya na Uingereza kufuatia kuenea kwa ugonjwa wa corona imeandaa kikao cha kwanza.
Kamati hiyo inayoongozwa na mwenyekiti mwenza Balozi Macharia Kamau ambaye ni katibu mkuu katika wizara ya mambo ya nje imeangazia maswala ya kiafya yanayoambatana na masharti hayo ya usafiri.
Taarifa hiyo imeeleza kwamba pande zote zimeangazia umuhimu wa kuwepo kwa haja ya Kenya na Uingereza kubaki na uhusiano wa karibu haswaa kibiashara ili biashara isitatizike.
Kamati hiyo ilibuniwa kufuatia mkutano wa kutuliza joto baina ya waziri wa mambo ya nje wa Kenya Balozi Raychelle Omamo na mwenzake wa Uingereza Dominic Raab.
Kenya ilikasirishwa na hatua ya Uingereza kuiongeza kwenye orodha ya mataifa yaliyoathirika zaidi na corona na kuwawekea raia wake vikwazo vya kuingia nchini humo.
Kenya ilijibu kwa kutangaza vikwazo zaidi kwa wanaosafiri kutoka Uingereza ikiwemo kujiweka kwenye karantini ya siku 14 na kulipia gharama yote.