Baada ya jaji Said Chitembwe, Profesa Kameri Mbote na jaji Martha Koome, ni zamu ya jaji David Marete Njagi kuwaelezea Wakenya ni kwa nini ana uwezo wa kuwa jaji mkuu mpya.

Jaji Njagi,62, ni mzaliwa wa kaunti ya Tharaka Nithi akiwa na uzoefu wa miaka 35 katika maswala ya sheria. Alikuwa wakili wa serikali katika afisi ya mwanasheria mkuu kwa miaka 17.

Alifanya kazi kama afisa mkuu wa maswala ya kisheria katika tume ya huduma za waalimu (TSC) kati ya mwaka 2003 na 2009.

Njagi aliteuliwa wakili wa mahakama ya kutatua mizozo ya kikazi mwaka 2012 ambapo amehudumu Nairobi, Kericho na Eldoret.

Akijitetea mbele ya tume ya huduma za mahakama JSC, jaji Koome ameelezea umuhimu wa kuwepo kwa haja ya mahakama ya upeo kutoa msimamo kuhusu hukumu ya kifo kwa sababu hukumu hiyo inaendelea kutolewa ilhali utafsiri wake haupo.

Jaji Koome ni mzaliwa wa mwaka 1960 kaunti ya Meru na ana uzoefu wa miaka 33 katika maswala ya kisheria tangu mwaka 1987.

Koome alijiunga na idara ya mahakama mwaka 2003 ambapo amekuwa akipanda ngazi kutoka mahakama kuu hadi mahakama ya rufaa.