Profesa Patricia Kameri Mbote amesema atatumia uzoefu wake katika maswala ya kisheria kuimarisha utendakazi wa idara ya mahakama iwapo atateuliwa kuwa jaji mkuu.

Profesa Mbote ambaye pia ni wakili amesema ana uzoefu wa kutosha kushikilia wadhifa huo kwa sababu amekuwa muhadhiri wa masomo ya kisheria tangu 2011 katika chuo kikuu cha Nairobi.

Ameahidi kutathmini mabadiliko yaliyoanzishwa na watangulizi wake Dkt. Willy Mutunga na David Maraga kufahamu yalikofikia kwa makusudi ya kujua ni vipi wataimarisha zaidi utendakazi wa mahakama.

Jaji wa mahakama kuu Said Juma Chitembwe alifungua ukurasa wa mahojiano hayo akisema ana uwezo wa kumrithi Maraga kwa sababu ya uzoefu wake katika idara ya mahakama.

Watu 10 wameorodheshwa kuhojiwa kwa wadhifa huo akiwemo majaji; Nduma Nderi, William Ouko, Martha Koome, Marete Njagi na mawakili Philip Murgor, Fredrick Ngatia, Moni Wekesa na Alice Yano.