Washukiwa watatu wa ujambazi wanaodaiwa kuwa miongoni mwa genge ambalo limekuwa likiwahangaisha watu katikati mwa mji Eldoret na viunga vyake wameuawa kwa kupigwa risasi Jumapili usiku.

Genge hilo la majambazi limekuwa likitekeleza wizi wa kimabavu katika siku za hivi karibuni ikiwemo kumuua Peter Kamau Njeri, mmiliki wa duka la jumla la Blessed Selection.

Wakati wa uchunguzi, Polisi waligundua kwamba majambazi hao walikuwa na mfumo mmoja wa kutekeleza uhalifu ikiwemo kujipanga katika genge la watu watano wakiwa wamejihami kwa bunduki aina ya AK-47.

Mara nyingi wamekuwa wakitekeleza uhalifu wao kuanzia mwendo wa 7:30pm kwa kujifanya kuwa wateja.