Wanafunzi kumi kutoka shule ya upili ya wavulana ya Anestar kaunti ya Nakuru wanazuiliwa na maafisa wa polisi kwa madai ya kujaribu kuingia ndani ya bweni la shule jirani ya wasichana ya Anestar Precious.

Taarifa kutoka idara ya upelelezi DCI inaeleza kuwa wanafunzi hao wa kike walipiga kamsa walipowaona wenzao wa kiume wakijaribu kuingia ndani ya bweni lao, na kuwalazimu maafisa wa polisi kutoka kituo cha Githioro kuingilia kati.

Hata hivyo wanafunzi hao wa kiume hawakusitishwa na uwepo wa maafisa wa polisi na walipokataa kuondoka, polisi wakafyatua risasi hewani kuwatawanya.

Haijabainika mara moja kiini cha wavulana hao kuingia katika bweni la wasichana na uchunguzi zaidi umeanzishwa.

Kumi hao wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Dundori huku wanafunzi wengine waliokuwa pamoja nao wakifaulu kutoroka.