Francis Atwoli amechaguliwa tena bila kupingwa kuendelea kushikilia wadhfa wa Katibu mkuu wa muungano wa vyama vya wafanyikazi nchini COTU.

Katika uchaguzi ulioandaliwa mapema leo, Atwoli mwenye umri wa miaka 71 amechaguliwa kuongoza COTU kwa muhula mwingine wa miaka mitano.

Kupitia kwa ukurasa wake wa Twitter, Atwoli ambaye amekuwa afisni tangu mwaka 2001 amewashukuru wajumbe wa muungano huo kutokana na imani yao kwa uongozi wake.

Atwoli ameahidi wafanyikazi wa humu nchini kuwa hatawasaliti katika utendakazi wake na kwamba atajitolea kuwatumikia kwa nguvu zake zote.

Katibu mkuu wa muungano wa wauguzi nchini KNUN Seth Panyako aliyekuwa anashindana na Atwoli kuongoza COTU alijiondoa dakika za mwisho.

Awali, Panyako na viongozi wa miungano nyingine ya wafanyikazi walikuwa wamemshtumu Atwoli kwa madai ya kutumia njia za mkato kusalia uongozini.