Naibu gavana wa Kilifi Gideon Saburi ameondolewa mashtaka ya kusambaza virusi vya corona kimakusudi mwaka jana.

Akitoa uamuzi huo, hakimu mkuu wa mahakama ya Mombasa Edna Nyaloti ameamuru kuwa Saburi hakutangamana na watu ili kuwaambukiza ugonjwa huo kwa hiari kwani wakati huo wizara ya afya haikuwa imetoa tahadhari ya kutosha.

Naibu huyo wa gavana alikuwa anashukiwa kutekeleza makosa ya kukiuka masharti ya usalama ya wizara ya afya kati ya Machi 6 na Machi 27 mwaka 2020 baada ya kurejea nchini kutoka kwa moja wapo ya mataifa yaliyokuwa yameripoti visa vya maambukizi ya corona.

Itakumbukwa kwamba mnamo Aprili 16, 2020, Saburi aliachiliwa kwa dhamana ya Sh200,000 pesa taslimu na hakimu mkuu Elvis Michieka na kuagizwa kusalimisha vyeti vyake vya usafiri mahakamani na asidhubutu kuhitilafiana na mashahid kwenye kesi hiyo.