Kenya na Uingereza wamekubaliana kuunda kamati ya pamoja kuangazia vikwazo vilivyowekwa na mataifa hayo mawili kuzuia msambao wa corona.

Uamuzi huo umeafikiwa kufuatia mazungumzo kwa njia ya simu baina ya waziri wa mambo ya nje Balozi Raychelle Omamo na mwenzake wa Uingereza Dominic Raab.

Pande zote mbili zimetaja mazungumzo hayo kama yaliyozaa matunda kiashirio kwamba mzozo wa kidiplomasia uliokuwa unanukia utasuluhishwashwa.

Maelewamo ya kubuni kamati ya pamoja yanawadia baada ya Kenya kukasirishwa na hatua ya Uingereza kuongeza Kenya kwenye orodha ya mataifa yaliyoathirika zaidi na corona na kuwawekea raia wake vikwazo vya kuingia nchini humo.

Kenya ilijibu kwa kutangaza vikwazo kwa wanaosafiri kutoka Uingereza ikiwemo kujiweka kwenye karantini ya siku 14 na kulipia gharama yote.