Miungano ya mashirika ya kijamii imekosoa serikali kutokana na mbinu inayotumia kupambana na maambukizi ya virusi vya corona.

Chini ya mwavuli wa Civil Societies Reference Group, viongozi wa miungano hiyo wakiongozwa na Suba Churchill wanasema serikali imepuuza washikadau wengine, hali ambayo inachangia ukaidi wa masharti ya kuzuia msambao wa virusi hivyo.

Katika taarifa iliyotiwa saini na Churchill, mashirika hayo yanaonya kuwa iwapo washikadau wengine hawatashirikishwa, wakenya wataacha kufuata masharti hayo pindi baada ya kaunti zilizofungwa kufunguliwa, hali ambayo italiweka taifa hatarini kukumbwa na wimbi la nne la maambukizi.

Churchil anataka serikali kutumia mashirika ya kijamii, viongozi wa dini na washikadau wengine kuhamasisha umma kuhusiana na umuhimu wa kuzingatia masharti ya kuzuia msmabao wa corona.