Raia wa Kenya wamepigwa marufuku kuingia nchini Uingereza kuanzia Ijumaa ijayo katika juhudi za taifa hilo kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.
Uingereza imeongeza Kenya kwenye orodha ya mataifa ambayo ni hatari zaidi kwa kuwa na virusi vya corona mengine yakiwa ni pamoja na Pakistan, Bangladesh na Ufilipino.
Katika taarifa, Ubalozi wa Uingereza hapa nchini umesema kuwa raia ambao wamekuwa Kenya kwa siku kumi zilizopita hawataruhusiwa kuingia kuanzia Aprili 10.
Mataifa mengine ambayo raia wake wamepigwa marufuku na Uingereza ni; Angola, Argentina, Bolivia, Botswana, Afrika Kusini, Brazil, Burundi miongoni mwa mengine.
Kenya kwa sasa inashuhudia wimbi la tatu la msambao wa virusi hivyo na kumlazimu rais Uhuru Kenyatta kukaza kamba katika utekelezwaji wa masharti ya usalama ikiwemo vikwazo vya usafiri katika kaunti tano zilizoathirika zaidi.