Mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Homabay Gladys Wanga amekosa kufika mbele ya tume ya uwiano na utangamano wa kitaifa NCIC kujibu tuhuma za kuzua vurugu akisema anasherehekea siku ya Wanawake.

Wanga katika barua ameitaka tume hiyo inayoongozwa na kasisi Samwel Kobia kumualika siku nyingine na wala sio leo Jumatatu kwa sababu ni siku ya kukumbuka mchango wa akina mama katika jamii.

Hata hivyo Wanga ameisuta tume hiyo ya NCIC kwa kukosa kuwachukulia hatua waliohusika na vurugu hizo wakati wa uchaguzi mdogo juma lililopita na badala yake kuwasingizia watu wasiokuwa na makosa.

Naye mbunge wa Kasipul Ong’ondo Were amefika mbele ya tume hiyo ila akokosa kuandikisha taarifa.

Mbunge huyo amesema mwaliko wake haukutaja makosa aliyofanya kwa hivyo ni lazima tume hiyo iwe bayana na makosa yake ili ajitetee.